
Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), profesa Ibrahim
Lipumba amekanusha taarifa kuwa yeye na Dk. Wilbroad Slaa wana mpango wa
kudhoofisha upinzani kutokana na uamuzi waliouchukua katika hatua za
mwisho.
Taarifa hizo zilieleza kuwa pamoja na mambo mengine, wawili hao wameamua
kuudhoofisha upinzani baada ya kunyimwa nafasi ya kugombea urais
kupitia Ukawa na badala yake nafasi hiyo alipewa Edward Lowassa
aliyetokea CCM.
Akiongea na Azam TV, Profesa Lipumba amesema kuwa wao ndio wapinzani
hasa na kuonesha jinsi walivyoumia kutokana na uamuzi wa Ukawa
kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais huku
wakiacha msingi wa hoja yao ya kupata katiba mpya.
“Wapinzani ni sisi, ukisema wapinzani ni sisi… mimi nimekuwa mwenyekiti
wa Chama Cha CUF toka mwaka 1999. Niliingia katika mapambano wakati kura
zimeibiwa Zanzibar, tumefanya maandamano nimevunjwa mkono, nikaibiwa
saa yangu na nimewekwa ndani,” alisema.
“ Sisi ndio wapinzani, wakati matukio haya yote yanatokea mheshimiwa
Edward Lowassa hakuwemo katika mapambano haya, kwahiyo hauwezi kusema
sisi tunavunja nguvu upinzani wakati sisi ndio vinara wa upinzani,”
aliongeza.
Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) siku
chache baada ya kushiriki katika kumpokea Edward Lowassa ndani ya Ukawa
akidai kuwa nafsi yake inamsuta.
No comments:
Post a Comment