Friday, September 4, 2015

MAJEMBE YALIYOKUZWA OLD TRAFFORD NA KWENDA KUPATA MAFANIKIO NJE YA JIJI LA MANCHESTER

Paul PogbaNa Salym Juma
Nikiamini wewe ni mzima wa afya, karibu sana katika ukurasa huu ambao unakupa habari za kuvutia kuhusu michezo mbalimbali inayoendelea kila siku ulimwenguni. Binafsi mimi ni mzima na leo nimejaaliwa kukuletea
wachezaji ambao walilelewa na Manchester United tangu wakiwa wadogo lakini baadae wamekwenda kupata mafanikio sehemu nyingine kabisa. Bila kukuchosha tazama wachezaji hawa hapa chini, karibu sana…..
RYAN SHAWCROSS 
Mchezaji huyu alizaliwa miaka 27 iliyopita kule Jijini Chester mpakani mwa nchi ya Wales na hatimaye mwaka 2002 alitimkia Old Trafford ambapo alianza maisha yake ya soka jijini Manchester  na kukaa klabuni kwa muda wa miaka sita kabla ya kwenda kutafuta maisha ya soka kule Royal Antwerp. Baada ya kukaa msimu mmoja kwenye klabu hii, hatimaye Stoke City walivutiwa na huduma ya mchezaji huyu na kumvuta Britania Stadium ambapo jezi namba 17 ilikuwa halali yake. Shawcross amekuwa muhimili mkubwa sana katika timu yake ya Stoke City kwa muda mrefu sasa.
Miongoni mwa mafanikio aliyopata nje ya Old Trafford ni pamoja na kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa klabu ya Stoke City kwa mwaka wa 2014. Inawezekana Ryan angeweza kucheza vyema kwenye idara ya ulinzi ya United kama angeaminiwa na kupewa nafasi hasa baada ya kupata uzoefu kwenye EPL kabla ya kusajiliwa na Stoke City mwaka 2008. Hadi kufikia hatua ya kuaminiwa na kupewa kitambaa pale Britania sio kitu chepesi kama watu wanavyodhani.
DANNY WELBECK
Ni vigumu sana kuamini kama ipo siku mchezaji huyu aliyekaa miaka 13 Old Trafford angeweza kuondoka United na kwenda London kwa mahasimu wakubwa wa Man U, Arsenal. Welbeck ni mchezaji anayeweza kukupa vitu viwili kwa wakati mmoja kwani hakuna asiyefahamu kuwa huyu ni kiungo mshambuliaji mzuri mbali na kuweza kucheza nafasi ya ushambuliaji ambayo mara kadhaa Sir Alex Fergurson alimchezesha.
Baada ya kuondoka United, Danny alifanikiwa kuwaonesha United kuwa hawakupaswa kumuachia kienyeji hasa pale alipofunga ‘hat-trick’ kwenye mechi ya ligi ya mabingwa dhidi ya Galatasaray. Pia Welbeck alifunga goli la ushindi na kuitoa nje ya mashindano ya FA timu yake ya zamani ya United. Inawezekana tatizo la safu ya ushambuliaji linaloikabili United kwa sasa lingepata suluhisho japo sio la moja kwa moja endapo Welbeck angebaki jijini Manchester.
RON-ROBERT-ZIELER
Huyu ni mlinda mlango kutoka taifa la Ujerumani na alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwakilisaha Ujerumani kwenye michuano ya kombe la dunia japokuwa hakucheza mechi yoyote. Ron alisajiliwa na United tangu mwaka 2005 kabla ya 2010 kwenda Hannover 96 ambapo alipata nafasi ya kuonesha kiwango chake. Kwa kipindi alichokuwa United, ilimuwia vigumu kuonesha kiwango chake hasa kutokana na ukweli kuwa akina Edwin Van Desar walikuwa na uhakika wa kucheza muda wote.
Inawezekana United wangethamini kiwango cha kinda huyu wasingehangaika sana kutafuta walinda milango wa kuziba nafasi ya De Gea endapo ataondoka. Ron ameiwakilisha Ujerumani katika ngazi zote za vijana kabla ya mwaka 2011 kuitwa rasmi kwenye timu ya taifa ya wakubwa.japokuwa hakuonekana kwenye kikosi cha kwanza kilichochukua ya kombe la dunia mwaka jana ila bado anajivunia kuwa miongoni mwa wachezaji waliovaa medali hiyo.
GIUSEPPE ROSSI
Kabla ya kwenda kwa mkopo Newcastle mwaka 2006, mchezaji huyu alikuwa pale Old Trafford tangu mwaka 2004 akiwa na miaka 17. United hawakuthamini kipaji chake na kufikia hatua ya kumtoa kwa mikopo
kwenye vilabu kadhaa vikiwemo vile vya Newcastle na Parma kabla ya
Villareal kunasa saini yake mwaka 2007 ambapo alikaa hapa kwa miaka takribani sita. Akiwa Hispania alifanya makubwa na hata Babu Fergurson kufikia hatua ya kutamani kumrudisha Old Trafford. Msimu wake wa kwanza mshambuliaji huyu alifunga magoli nane kwenye UEFA na kuanza kutiliwa mashaka na mabeki kibao.
Miongoni mwa mafanikio aliyoyapata nje ya United ni yale ya kufunga magoli 32 kwenye mechi 56 alicheza pale Villareal. Pia baada ya kuhamia Fiorentina, Rossi alifunga magoli 14 ndani yamechi 18 alizocheza licha ya majeruhi kumuandama mara kwa mara. Japokuwa anapata majeraha ya mara kwa mara, Rossi bado ameiwakilisha timu yake ya taifa mara 30 na kufunga magoli 7 huku muda mwingi akitokea benchi.
GERALD PIQUE
Miongoni mwa wachezaji waliopata mafanikio hasa baada ya kuondoka Old Trafford ni ‘Baba Shakira’ Huyu jamaa licha ya kusajiliwa kwa mkopo Real Zaragoza, bado alikuwa anamilikiwa na United kabla ya kusajiiwa na Barcelona mwaka 2008. Pique hakuonekana sana pale United kutokana na uwepo wa John Oshea na makosa yake madogo madogo ambayo hadi leo yanaonekana pale Camp Nou.  Wachambuzi wengi wa soka walitegemea Pique lazima angeondoka Old Trafford hasa baada ya Fergurson kutovutiwa sana na uchezaji wake.
Tunapozungumzia mafanikio aliyoyapata Gerald Pique baada ya kumpa mkono wa kwaheri Sir Alex Fergurson, ni yale ya kuchukua vikombe kibao akiwa na Barcelona, vikombe ambavyo asingevipata kama angebaki nchini Uingereza. Pique pia amefanikiwa kuiwakilisha vyema timu yake ya taifa hadi kuchukua kombe la dunia na lile la Euro. Mafanikio haya ameyapata baada ya kucheza kwa mafanikio pale FC Barcelona na hatimaye kuaminiwa na kocha wa timu ya taifa ya Hispania.
PAUL POGBA 
Nina uhakika Manchester United wanajuta hadi leo pale wanapomuona Pogba akifanya yake katikati ya uwanja. Kiungo huyu muhimu alikaa kwa muda wa miaka 2 pale kwenye Academy ya Manchester United kabla ya kupandishwa kwenye timu ya wakubwa mwaka 2012. Hatimaye Juventus walinasa saini yake na kumpa nafasi ya uhakika kikosini kitu ambacho kilimfanya aiwakililishe Ufaransa kwenye ngazi zote za vijana na hata
timu ya taifa ya wakubwa. Hakuna anayebisha juu ya kiwango cha mchezaji huyu anayewindwa na timu za Chelsea na FC Barcelona. Mafanikio aliyopata baada ya kuondoka pale United ni makubwa mno kulingana na umri wake. Nadhani mnakumbuka kwenye michuano ya kombe la dunia iliyomalizika mwaka jana ambapo Pogba alichukua tuzo ya Mchezaji bora chipukizi wa michuano hiyo. Kama hiyo haitoshi, Pogba pia  baada
ya kuisaidia Juventus kufika fainali ya UEFA, hatimaye alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi pia. Usishangae kuona dirisha lijalo Pogba akavunja rekodi ya usajili kwa kuchukuliwa na Chelsea au Barcelona.

No comments:

Post a Comment

Popular Posts