Monday, August 31, 2015

KIIZA AHITIMISHA WAKATI SIMBA IKIINYUKA MAFUNZO YA ZANZIBAR

Hamisi Kiiza 'Diego' (kulia) akijaribu kumtoka mchezaji wa Mwadui wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa kirafiki hivi karibuni
Hamisi Kiiza ‘Diego’ (kulia) akijaribu kumtoka mchezaji wa Mwadui wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa kirafiki hivi karibuni
Baada ya jana kubanwa na kupokea kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa JKU, hatimaye Wekundu wa Msimbazi leo wameibuka na ushindi wa goli 3-1 walipocheza mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar ambayo ndio mabingwa watetezi wa ligi kuu ya visiwani Zanzibar.
Mchezo huo ulisukumwa saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Amaan, Mafunzo ndio walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Simba kipindi cha kwanza dakika ya 30 kupitia kwa Jaku Juma akitumia vizuri pasi iliyopigwa na Haji Ramadhani na kuukandamiza mpira wavuni.
Simba wakasawazisha bao hilo dakika ya 36 mfungaji akiwa ni Peter Mwalyanzi, bao la pili la Simba limefungwa na Said Issa kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Awadh Juma dakika ya 43.
Hamisi Kiiza ‘Dioego’ aliifungia Simba goli la tatu na la ushindi dakika ya 68 akitumia vyema pasi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto aliyeshirikiana na Mussa Mgosi kupika bao hilo.
Simba ipo visiwani Zanzibar kwa kambi ya mwisho ya maandalizi kuelekea michuano ya ligi kuu inayotarajia kuanza kurindima kuanzia Septemba 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Popular Posts