Tuesday, September 8, 2015

UUNGWANA NA UHAMASISHAJI NJE YA UWANJA VINAWAFANYA WACHEZAJI HAWA KUWA MIFANO YA KUIGWA

Demba-BaNa Salym Juma
Busara, uungwana na uhamasishaji ni vitu muhimu sana ambavyo binafsi naota kuwa navyo muda wote wa maisha yangu. Nelson Mandela na Julius Nyerere wanaweza kukaa katika kipengele hiki kwa upande wa siasa. Kwa Wanasiasa wa karibuni nashindwa kuwatambua moja kwa moja ni akina nani hasa wana busara ila piga ua Mzee James Mbatia siwezi kumuacha. Katika soka pia wapo wachezaji wenye sifa hizi na wanapaswa kuwa mifano ya kuigwa na watu wote duniani. Leo hii nimejaaliwa kukuletea wachezaji wachache ambao ni mifano ya kuigwa nje na ndani ya uwanja kutokana na matendo yao, karibu sana…
DIDIER DROGBA
 Chelsea inamkumbuka zaidi kwenye fainali ya UEFA pale Munich. Nje ya uwanja huyu jamaa ni muungwana sana kwani utakumbuka
mwaka 2006 jinsi alivyoiunganisha nchi yake kwa kuyaomba makundi yote yenye silaha kuweka silaha chini na kuwa kitu kimoja. Pia Drogba ana kituo chake cha kutoa misaada kinachoitwa ‘Didier Drogba Foundation’. Vyote hivi Didier anavifanya ili kuwasaidia binadamu wa kawaida kabisa nje ya soka na kwa kiasi fulani amefanikiwa sana katika hili na Mungu anazidi kumpa riziki. Ndani ya uwanja pia Drogba mara kadhaa ameonekana kuwapa moyo wachezaji wadogo.
LIONEL MESSI
Ni vigumu sana kumuacha huyu jamaa pindi unapozungumzia wachezaji waungwana tena wenye vitendo vya kistaarabu. Messi baada ya kugundua kuwa yeye ni Njiti alikuwa anadungwa sindano moja kila siku matibabu ambayo yaliigharimu familia yake Dola 1500 kwa mwezi. Familia
yake haikuweza kumudu gharama hizi na ilimlazimisha Messi kwenda Barcelona ili aweze kukidhi gharama hizi. Mbali na suala hilo, pian Messi mara kadhaa alionekana kukataa tuzo ya mchezaji bora wa mechi kwa kuamini kuwa hakustaili. Pia aliwahi kumpa Neymar mkwaju wa penati licha yeye kuhitaji goli 1 ili afunge ‘hat-trick’
ANDRES INIESTA
 Mbali na upole wake nje na ndani ya uwanja, Iniesta pia ni miongoni mwa wanasoka wa kuigwa. Wahispania wanamkumbuka zaidi pale alipofunga goli kwenye fainali ya kombe la dunia mwaka 2010. Akiwa kwenye ndege njiani kuelekea South, Iniesta aliamka kwenye siti na kuweka DVD ambayo ilionesha jinsi nchi ya Hispania ilivyoshindwa kwenye vita na hatimaye kurejea tena na kushinda vita kwa kishindo. Kitu hichi kiliwapa moyo sana wachezaji wenzake na hatimaye walichukua ubingwa. Pia Iniesta amekuwa akiwatuliza wachezaji wenzake pindi vurugu zinapotokea uwanjani.
MIROSLAV KLOSE
Inawezekana busara na uungwana wake umemsaidia kuwa mfungaji bora wa kombe la dunia hadi sasa. Akiwa Werder Bremen mwaka 2005, Mwamuzi alitoa penati baada ya golikipa wa Bielefeld kuonekana kamchezea faulo Klose. Baada ya filimbi, Klose alimfata Mwamuzi na kumwambia kuwa Golikipa ndio alikuwa wa kwanza kuugusa mpira. Akiwa Lazio pia wakati timu yake inacheza na Napoli, Klose alifunga goli la kuongoza kwa kichwa baada ya mpira wa kona. Klose alimwambia Mwamuzi kuwa alikuwa ameugusa mpira kwa mkono na siyo goli. Baada ya mchezo Lazio walilala 3-0. Klose alipongezwa kwa uungwana huu.
DEMBA BA
Ni miongoni mwa wachezaji wapole na waungwana nje na ndani ya uwanja. Uchamungu wake umemsaidia kutekeleza matendo kibao ya kiungwana kwani mara kibao ameonekana akisaidia masikini kule kwao Senegal. Tukio lingine la kukumbukwa ni lile la kujenga Msikiti kule kwao na kufuata nyayo za Frediric Omar Kanoute aliyenunua Msikiti pale Seville wakati anacheza soka la kulipwa Spain. Demba Ba akiwa nje ya uwanja anapenda kushinda na familia yake huku akiwaza ni jinsi gani atawasaidia watu wasiojiweza.
Vipi kwa mtazamo wako nani katisha zaidi miongoni mwa hawa wachache kati ya wengi wenye matendo yanayofanana na haya? Naamini huu ni muda wachezaji wetu na watu wengine maarufu kuiga vitu kama hivi, huu mtazamo tu lakini.

No comments:

Post a Comment

Popular Posts