WAKATI kiongozi wa Chama cha ACT
Wazendo, Zitto Kabwe, ameomba Watanzania waruhusiwe kuingia bure
uwanjani kuishangilia Taifa Stars dhidi ya Nigeria keshokutwa Jumamosi,
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vikubwa kwa
ajili ya mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika
(AFCON) 2017.
Wakati wa uzinduzi wa kampeni za
chama hicho kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu zilizofanyika Mbagala jijini
Dar es Salaam Jumapili, Zitto alishauri TFF iruhusu mashabiki waingie
bure kwenye Uwanja wa Taifa kuipa sapoti kubwa timu ya nyumbani.
Hata hivyo, katika mkutano na
waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo, Baraka
Kizuguto, ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, ametangaza
kiingilio cha chini ya Sh 7,000 huku akimjibu kwa kifupi Zitto kwa
kusema: “Tusichanganye siasa na michezo”.
Kizuguto amesema maandalizi ya
mechi hiyo ya Kundi G yamekamilika huku akieleza kuwa kiingilio cha juu
(VIP A) Sh 40,000, VIP B Sh 30,000, VIP C Sh15,000, Rangi ya Machungwa
Sh 10,000 wakati viti vya rangi ya Bluu na Kijani Sh 7,000.
Amesema tiketi za mchezo huo
zinatarajiwa kuanza kuuzwa leo saa 4 asubuhi katika vituo 10; Ofisi za
TFF, Buguruni, Mbagala, Ubungo, Makumbusho, Uwanja wa Taifa, Mwenge,
Kivukoni, Posta (Luther House) na Kariakoo (Msimbazi).
Amesema mechi hiyo itakayoanza
saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, itachezeshwa na waamuzi
kutoka Rwanda ambao wanatarajiwa kuwasili jijini leo jioni.
Marefa hao ni Louis Hakizimana
(kati), Honore Simba (msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (msaidizi) na
Abdoul Karim Twagiramukiza (wa akiba) pamoja na kamisaaa Charles Kasembe
kutoka Uganda.
No comments:
Post a Comment