Ivo (kulia) alikuwa mwalimu mzuri wa Manyika Peter Jr (kushoto)
Wekundu wa Msimbazi Simba SC,
rasmi wameachana na golikipa wao mkongwe, Ivo Philip Mapunda wakidai
kwamba hakutoa ushirikiano wakati alipotakiwa kusaini mkataba mpya.
Taarifa zilieleza kwamba Ivo
alikabidhiwa Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuanguka mkataba mpya,
lakini hajatokea licha ya kutafutwa na viongozi wa Simba.
Ivo amekiri kutopewa mkataba na uongozi wa Simba baada ya kuonana nao kwa mazungumzo zaidi.
“Nimeambiwa sikuonyesha
ushirikiano wakati natakiwa kwenda kusaini fomu, wamesitisha mkataba
kwasababu hiyo, wanadai kiongozi aliyepewa jukumu hilo alinitafuta sana
na akapeleka taarifa kwamba sitoi ushirikiano, kwahiyo hawajanipa”.
Amesema Ivo.
Hata hivyo imeelezwa kwamba
viongozi wa Simba wamemtaka mlinda mlango huyo kurejesha fedha
alizochukua ambazo zinadaiwa kuwa milioni 10.
“Nimeambia nirejeshe fedha
nilizochukua, mimi nimesema sawa, sihitaji mgogoro, nataka nitoke Simba
salama, kama wao wanahitaji nirudishe pesa yao, nitarudisha”. Amefafanua
Ivo na kuongeza: “Nilipochukua pesa nilifanyia biashara, pale
nitakapoipata nitarudisha, lakini siwezi kusema nitarudisha lini”.
Je, ni kweli alichukua milioni
10?Ivo amesema: “Siwezi kusema ni shilingi ngapi, siwezi kuweka mambo
hadharani, hayo ni maneno tu, mimi ninachosema ni kwamba nitarudisha
nitakapoipata”.
“Kitu kizuri inatakiwa usiwe mropokaji, nitakapoipata nitarudisha, labda kitu ninachoweza kuwa muwazi ni kwamba sina kinyongo”
“Nawashukuru sana wanasimba,
walinipa sapoti nilipokuwa nafanya vizuri na vibaya, nawatakia kila la
kheri, katika maisha ya mpira, mlango mmoja ukifungwa mwingine unakuwa
wazi”
Nao Simba wamekiri kuachana na Ivo baada ya kushauriana na kocha wa makipa.
Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Simba, Haji Manara amesema: “Kimsingi tulikuwa na kikao
kizuri na cha kuungwana na Ivo, baada ya kushauriana na mwalimu wa
magolikipa, kocha ameridhika kabisa na uwezo wa magolikipa waliopo kwa
maana ya Vicent Angban kutoka Ivory Coast na magoli wetu chipukizi Peter
Manyika na Dennis Richard. Ivo tumeachana naye kwa amani”.
“Kuhusu kuambiwa kurejesha
fedha, mimi sijaambiwa taarifa hiyo na viongozi. Kama Ivo kasema hivyo,
hiyo inaweza kuwa taarifa rasmi, ila mimi sijaambiwa”. Amesema Manara.
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Baada ya miaka miwili na nusu
kuichezea Simba SC hatimaye golikipa Ivo Mapunda ataondoka katika klabu
hiyo baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Ivo, golikipa wa zamani wa timu
ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na klabu za Tukuyu Stars, Tanzania
Prisons, Moro United, Yanga SC, St.George ya Ethiopia, African Lyon
alijiunga na Simba, Desemba, 2013 akitokea Gor Mahia FC ya Kenya
alifanya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya kabla/baada ya kumalizika
kwa ligi kuu msimu uliopita lakini Jumatatu hii klabu.
Ivo alisajiliwa Simba ili
kusahihisha makosa ya mlinda mlango, Mganda, Abel Dhaira ambaye kwa
mtazamo wangu ndiye kipa ‘ dhaifu’ zaidi kuwahi kuichezea timu hiyo
katika kipindi cha miaka 15 sasa.
Dhaira alisainiwa kama mbadala wa
aliyekuwa kipa namba moja wa muda mrefu, Juma Kaseja wakati wa usajili
wa dirisha dogo, Desemba, 2012.
Mganda huyo alikuwa akitoka hovyo
golini huku akitema mipira mara kwa mara, nakumbuka alifungwa mabao ya
kizembe katika sare ya Simba 2-2 na Mbeya City, Septemba, 2013 wakati
alipofungwa goli la mbali na Paul Nonga.
Pia, Dhaira ndiye mchezaji
aliyedaka katika sare ya Yanga 3-3 na Simba, Oktoba, 2013 na baada ya
mechi hiyo mashabiki wakahitaji mabadiliko ambayo yalishuhudia IVO
akitua katika timu hiyo huku akiwa mshindi wa ligi kuu ya Kenya.
Akiwa ametoka kufanya vyema
katika michuano ya Cecafa Challenge Cup nchini Kenya, Ivo alikataa
kusaini mkataba mpya na Gor na kuamua kurejea nyumbani na kwa mara ya
kwanza tangu mwaka 2007 akashiriki katika pambano la mahasimu wa soka
nchini, Yanga na Simba katika mchezo wa Hisani wa Nani Mtani Jembe-1,
2013. S
imba ilishinda 2-0 huku IVO
akicheza kwa kiwango cha juu. Dhaira akaondoka zake na mara baada ya
kumalizika kwa msimu wa 2012/13 baada kuwa msugua benchi.
Mtibwa Sugar 1-1 Simba SC, Mgambo JKT 2-1 Simba SC, Simba SC 1-2 Kagera Sugar….
Mechi hizi Tatu hakika Ivo
hatazisahau. Akiwa ameanza vizuri katika Mtani Jembe, kipa huyo
aliendeleza kiwango cha juu hadi alipokuja kuruhusu bao la umbali mrefu
wakati timu yake ilipocheza na Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri,
Morogoro katika mchezo wa ligi kuu, Februari, 2014. Musa Hassan Mgosi
alipiga mpira mrefu ‘ kama krosi’ ambayo ilisogwa na upepo na kuelekea
golini kwa kasi. Mpira huo ulimshinda Mapunda na kutinga nyavuni.
Siku chache baadaye Mapunda
alilaumiwa wazi na mashabiki wa klabu ya Simba baada ya kufungwa goli
rahisi katika mchezo ambao Simba ililazwa 2-1 na Mgambo JKT katika
uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Hizo zilikuwa mechi mbili ambazo, Ivo
zilianza ‘ kumuweka njia panda’. Ilikuwa ni katika michezo ya mzunguko
wa pili msimu wa 2013/14.
Msimu wa 2014/15 Simba ilikuwa na
magolikipa watatu, Ivo Hussein Shariff ambaye alisajiliwa akitokea
Mtibwa huku mkono akiwa na tuzo ya kipa bora wa ligi kuu ya Vodacom
msimu wa 2013/14, pia alisajiliwa kijana wa timu ya Taifa ya Vijana ya
Tanzania, Manyika Peter Manyika ‘ Manyika Jr’.
Ivo ambaye tayari alikuwa
amecheza gemu mbili mfululizo ya ‘ Dar es Salaam derby’ na kuruhusu
nyavu zake mara moja akaendelea kuwa kipa chaguo la kwanza cha Mzambia,
Patrick Phiri hadi pale aliporuhusu magoli mawili ya ‘ kizembe’ katika
kipigo cha Simba 1-2 Kagera Desemba, 2014 katika uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Alidaka vizuri katika mchezowa Mtani Jembe-2. Gemu ambayo Simba
iliishinda Yanga 2-0.
Baada ya kutishia kuachana na
klabu hiyo mara baada ya kusakamwa sana kufuatia kuruhusu magoli rahisi
aliyekuwa mwalimu wa timu hiyo, Phiri aliwajibu baadhi ya viongozi na
mashabiki wa timu hiyo kuwa hawapaswi kumlaumu Ivo bali wamlaumu yeye
ambaye alimpatia amliptatia nafasi ya kucheza.
Manyika akapangwa kwa mara ya
kwanza katika mchezo wa Simba 0-0 Yanga, oktoba , 2013 baada ya Ivokuwa
na majeraha ya kidole huku Shariff akiwa na majeraha makubwa ya mguu.
Kijana huyo ambaye alikuwa akiichezea Simba kwa mara ya kwanza aliweza
kufanya vizuri kiasi cha kutajwa kama mrithi wa kweli ya Kaseja, lakini
baada ya muda mfupi Manyika akapoteza nidhamu kiasi cha kudili zaidi na
watu waliokuwa wakimkosoa na kuachana kuwekeza mkazo katika kurekebisha
makosa yake ya kutoka hovyo langoni.
Ivo alipona na kuanza kushindania
namba na Manyika na kushinda vita hiyo. Atakumbukwa kwa mipambano minne
aliyocheza dhidi ya Yanga kwani alikuwa kama ‘ hirizi ya bahati’ ya
klabu ya Simba kwani katika gemu Tano za mwisho za mahasimu hao wa soka
nchini zimeshuhudia Yanga ikifunga mara moja tu. Mechi ya mwisho kwa Ivo
ambayo pia ilikuwa ni ya nne kwake ilikwisha kwa Simba kushinda 1-0
Machi mwaka huu katika VPL.
Ivo anaondoka Simba akiwa shujaa
anayechukiwa kisirisiri kwani ameshinda mataji mawili ya Mtani Jembe,
Moja la Mapinduzi Cup huku akiwa ameshinda mechi tatu kati ya Nne
alizocheza dhidi ya Yanga SC. Mechi Tatu alizobonga kwangu haziwezi
kufuta sifa yake nzuri ya uaminifu kwa klabu ya Simba, alichezea kwa
moyo na kama mchezaji wakati mwingine alifanya makosa. Ivo si Shujaa wa
Simba Pekee, ameshinda VPL 2 akiwa Yanga, Ubingwa wa ligi kuu ya
Ethiopia na Kenya alikuwa shujaa kwa mashabiki wanazi wa Gor….