Na Salym Juma
Asee haya mataifa ya Ulaya
yananifurahisha sana eti leo yanalalamika kuhusu wimbi la wahamiaji
haramu kupitia Libya wakati wao ndio chanzo cha haya yote. Muammar
Gaddafi alipokuwa imara ni nani aliyekatiza Libya kuingia Ulaya
kirahisi? Tena bado tegemeeni pia wahamiaji wengine kibao kutoka Yemen
na Syria maana nyie ndo chanzo cha yanayoendelea Mashariki ya Kati. Eti
unakuta nchi ya Amerika na Ulaya zinaoongoza kuuza mafuta, jiulize
wanatoa wapi? Ugaidi duniani kuisha ni ngumu sana maana kuna mambo kibao
yaliyojificha zaidi hata ya zile chaguzi za DRFA. Anyway tugeukie
kwenye soka maana binafsi napata hasira sana nikizitazama sera za nje za
mataifa ya Magharibi.
Katikati ya wiki hii macho na
masikio mengi yalielekea pale Monaco, sehemu ambapo ‘Draw’ ya kupanga
makundi nane yenye timu 32 ilikuwa inafanyika, mbali na mchawi Messi
kutajwa kama mchezaji bora wa Ulaya kwa mara ya pili, kitu kingine
kilichoteka watu ni kitendo cha kundi la D kuwa na timu zenye msimu
mzuri ama kwa lugha ya vijana wanasema zipo‘Onfire’. Kundi hili lina
timu za Juventus, Manchester City, Sevilla na ndugu zangu Borussia
Monchengladbach. Kwa wale wapenzi wa soka, kundi hili sio la kifo bali
ni zaidi ya kifo. Naamini yapo mengi ya kutazama juu ya kundi hili.
Kwa wale ndugu zangu ambao
tunapoteza muda wetu mwingi kufuatilia habari za michezo hususani soka,
mtaungana na mimi kuwa tangu waarabu wamwage pesa pale Etihadi, Man City
ilirejea kwenye michuano ya Ulaya ila imekuwa ikikwamishwa na timu
kutoka mataifa matatu, Hispania, Ujerumani na Italia. Msimu huu pia City
imekutana na timu kutoka mataifa haya kwenye hatua za mapema kabisa.
Ungana nami hadi mwisho wa makala hii kutathmini kundi hili hatari
kabisa pengine kuliko makundi mengine saba. Karibu sana…..
Manchester City baada ya
uwekezaji wa kutosha tangu kuondoka kwa Mark Hughes, City ilifika
fainali ya kwanza tangu miaka 30 kupita kwa kuchea fainali ya FA mwaka
2011. Kwa mara ya kwanza tangu 1968, City ilirejea kwenye ligi ya
mabingwa barani Ulaya mwaka 2011 na kujikuta inapangwa na Bayern Munich,
Villarreal na Napoli. Man City walishindwa kuifunga Napoli kwenye mechi
ya ufunguzi na hatimaye baada ya vipigo kutoka kwa Napoli na Bayern
Munich, City walishika nafasi ya 3 baada ya Villarreal kuonekana vibonde
na hii ndo ilikuwa safari ya mwisho ya City kwenye makundi.
Msimuu wa 2012-13, Manchester
City kama ilivyo kawaida ilikutana tena na Wajerumani na Wahispania
japokuwa safari hii Wataliano hawakuwepo. Real Madrid na Borussia
Dotmund walipangwa kundi moja na City huku Ajax akifunga hesabu ya
kundi. Man City ilionewa sana kipindi hiki kwani hata nafasi ya kucheza
Europe league hawakuipata baada ya kushika mkia nyuma ya Ajax. City
hawakushinda mechi hata moja licha ya kuwa wababe kwenye Epl kwa kipindi
hiki, walitoa sare tatu huku wakipoteza mara tatu na kuruhusu magoli ya
kutosha.
Msimu wa 2013-14, mzimu wa
Kijerumani ulizidi kuwaandama City kwa mara nyingine hasa baada ya
kupangwa tena na Wajerumani. Kipindi hiki walipangwa na Bayern Munich
huku Victoria Plzen na CSKA Moscow wakikamilisha kundi. City ilijitahidi
baada ya kuwaonea vibonde hawa wawili na hatimaye kumaliza nyuma ya
Bayern baada ya kutoa vipigo vitano na kupoteza mara moja. Mzimu wa
Kihispania haukuwaacha City kwani walipata kipigo kitakatifu cha 4-1 na
kutolewa na FC Barcelona kwenye hatua ya 16 bora. Hapo Wahispania na
Wajerumani waliikwamisha tena City.
Msimu uliopita City walikutana
tena na Wajerumani na Waitaliano. Bayern Munich na AS Roma ndio timu
zilizoingia kwenye kundi moja na City huku CSKA Moscow wakikamilisha
kundi la nne. City walifanya upuuzi sana japokuwa walifuzu 16 bora kwani
walishinda mechi mbili pekee huku wapinzani wao Roma na CSKA wakishinda
mechi moja moja. Kama kawaida Wahispania waliwakwamisha tena City baada
ya Barcelona kuwatoa kwenye raundi ya 16 bora kwa jumla ya magoli 3-1.
Ukijaribu kutazama safari yao tangu kurejea kwenye UEFA wamekuwa
wakikwamishwa na Wajerumani, Wataliano na Wahispania.
Juventus ni timu nyingine ya
Italia ambayo imepangwa na City msimu huu. Juventus ni mabingwa wa
Italia na makamu bingwa pia wa Kombe hili. Ukijaribu kukiangalia kikosi
cha Juventus licha ya kuondokewa na wachezaji wake muhimu ila kuna kitu
kimoja kinaitwa ‘uzoefu’ wa michuano ya Ulaya. Juve ni miongoni mwa timu
zenye vikosi vipana kidogo pale Italia tofauti na timu nyingine,
kutokana na hili usishangae ikachukua pointi 4 kwenye mechi 2 itakazo
kutana na Man City. Wengi tunajua kuwa City ni wazuri ndani ila nje ni
wa kawaida sana na hili litazidi kutokea tena.
FC Sevilla ni timu nyingine
iliyopangwa na City kundi moja. Kumbuka hawa ni mabingwa wa Europe
league na shughuli yao Barcelona wanaijua.Nitakuona wa ajabu kama
ukiniambia City itachukua pointi yoyote pale Estadio Ramon Sanchez
Pizjuan watakapokutana na FC Sevilla. Hata pale watakapoikaribisha
Etihad bado itakuwa ngumu kuwafunga Wahispania hawa ambao wamekuwa
tishio kubwa sana kwa timu za Barcelona na Real Madrid kwenye La liga.
Sevilla wapo vizuri sana wanapokutana na timu za kizembe na usishangae
kuona wanachukua nafasi 2 za juu kwenye kundi hili gumu.
Wajerumani wengine watakao ongeza
gundu kwa City ni Borussia Monchengladbach, vijana wa pale Stadionim
Borussia Park chini ya kocha wao Lucien Favre. Monchengladbach
walimaliza nafasi ya tatu kwenye ligi ngumu ya Bundesliga msimu
uliopita. Walitolewa kwenye hatua za awali za michuano ya Europe league
msimu uliopita ila shughuli yao ilionekana kwenye Bundesliga. Msimu huu
wameanza vibaya baada ya kikosi chao kutotulia ila bado itakuwa sio kazi
rahisi kwa City kuchukua pointi pale Ujerumani mbele ya mashabiki 54,
000 wa Monchenglabach. Inawezekana Monchengladbach ikapoteza mechi
nyingi za ugenini kutokana na kutokuwa wazuri nje ya Ujerumani ila kwa
mechi tatu za ndani isipoteze mechi hata moja.
Kwa ujumla mbinu mbadala za
Manuel Pellagrin na kuwaandaa wachezaji wake Kisaikolojia ndicho kitu
ambacho kinaweza kuwasaidia kumaliza kwenye nafasi mbili za juu katika
kundi hili la kifo. Juventus kwenda kuchukua pointi moja Hispania, moja
Ujerumani na ttu pale Etihad ni kitu cha kawaida sana kama City
hawatojipanga vizuri. Pia Sevilla kwenda kuchukua pointi moja pale
Etihad na tatu Ujerumani ni kitu cha kawaida kabisa. Bila shaka City
inapaswa kushinda mechi zote za nyumbani au hata kukusanya pointi saba
kati zile tisa za nyumbani, wakifanya hivi watakuwa wamemaliza kazi
mapema sana.
Mwisho wa siku japokuwa soka ni
mchezo wa makosa na huwezi kutabiri mpira wa miguu kwani maajabu yana
nafasi yake ila inawezekana kundi hili likamtoa mshindi wa kwanza akiwa
na pungufu ya pointi 12 huku magoli ya kufunga na kufungwa yakiamua nani
asonge mbele nani abaki Europe league na nani ashike mkia. Manueli
Pelagrin anapaswa kuchanga karata zake vyema ili asije kuaibika kwa mara
nyingine tena kwenye michuano hii mikubwa kabisa katika ngazi ya Ulaya
barani Ulaya. Yetu macho tuu na ‘Inshaa Allah’ tutajaaliwa uzima na
kushuhudia kila kitu kwenye kundi hili.
No comments:
Post a Comment